Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wabunge wa CCM, epukeni fikra zilizoganda

15th July 2012
Print
Comments

Nianze kwa kuweka wazi kwamba sina chuki na Mbunge yoyote anayetokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa maana wapo kwa mujibu wa haki za binadamu na misingi ya demokrasia. Wanaistahili heshima yao.

Ninatambua wazi kwamba wapo wabunge wanaotokana na chama hicho ‘kilichozaliwa’ Februari 5, 1977 pale mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, wanaoujua, kuuishi na kuutetea wajibu wao kwa umma.

Kwamba wana wajibu binafsi, wana wajibu kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wana wajibu kwa vyama vyao vya siasa, wana wajibu kwa wapiga ndani ya majimbo yao ya uchaguzi. Haipingiki.

Lakini wapo wabunge ambao nadiriki kuweka wazi kwamba ni wanachama wa CCM, waliochaguliwa kutokana na tiketi ya chama hicho, lakini wanashindwa kutimiza sehemu ya wajibu huo.

Si kwamba wabunge kupitia CCM peke yake wana upungufu katika kutimiza wajibu wao, la hasha. Wapo hata ndani ya vyama vya upinzani ingawa ni kwenye maeneo tofauti. Ninajadili.

Tangu kuanza kwa vikao vya Bunge la bajeti, umma umewashuhudia wabunge kupitia CCM wakijiweka pembeni ya maslahi ya umma, wakijivua ‘koti’ la kuwa wajumbe wa mhimili unaopaswa kuisimamia na kuishauri serikali, wanakuwa wasemaji wa serikali.

Ni kweli kwamba serikali iliyopo madarakani imeundwa na Rais Jakaya Kikwete anayetokana na CCM. Sehemu kubwa ya watendaji wake lazima watokane na wanaoiishi itikadi ya chama hicho, hata kama dhamira, nia na utashi wao haviridhishwi na mwenendo wa CCM.

Inawezekana kwa dhana hiyo, ndiyo maana wabunge wanaotokana na CCM (kwa idadi isiyokuwa rasmi) wanajisahau ama kuwa mfano wa mtu aliyejivisha shuka nyeupe asiione nuru, wanashindwa ‘kujivua gamba’ la u-CCM pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kibunge.

Katika kipindi hicho, wabunge wa aina hiyo, badala ya kuihoji serikali, wamegeuka kuwa wasemaji wake. Wanatoa majawabu yaliyopaswa kutolewa na wawakilishi wa serikali bungeni, yaani mawaziri.

Ni wingi zito limetanda! Mbunge anapoamua kuwa msemaji wa serikali, si rahisi kumtofautisha na mzazi mwenye mtoto anayekiuka maadili mema, akavaa `mivao’ ya ajabu, akavuta bhangi, akatumia dawa za kulevya, akajiuza mwili akitafuta wateja kando kando ya barabara, kisha akamsifia (eti) kwa sababu ni mtoto wake.

Mzazi wa aina hiyo anaweza kuona soni na kutaka aonekana mwenye kuitunza familia yenye amani, umoja na mshikamano, lakini mtoto akiendelea kuharibika, kuichafua sifa njema ya familia na kila ‘anapoguswa’ kwa kukosolewa, mzazi anakuja juu, anamlinda.

Wabunge hususani wa upinzani wanapoibua hoja zenye kuikosoa serikali inaposhindwa kufikia matarajio ya umma, wanakuwa mfano wa mzazi mwenye sifa na hulka niliyoitaja, nikiwa sina nia mbaya dhidi yao.

Kwa maana kama serikali inashindwa kufanikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, maji safi na salama, elimu na nyingine zinazotegewa katika kuchagiza kasi ya maendeleo ya nchi na ustawi wa watu wake, kuna maana kwa mbunge ‘kuikingia kifua’ eti kwa sababu tu inatokana na chama chake?

Inafikia hatua kubwa zaidi, kwamba wakati wana-CCM wakiwemo wabunge wake, walisimama majukwaani wakielezea mpango wa kisayansi utakaotumika kuharakisha kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, maarufu kama Ilani ya Uchaguzi, baadhi ya watendaji serikalini wanaonekana kwenda kinyume.

Wakiwa wamepewa jukumu la kuzitumia rasilimali za umma kwa ajili ya kuustawisha umma, wao wanajilimbikizia na pengine wanazihujumu rasilimali hizo, bado mbunge wa CCM anasimama kusimamia uozo huo! Inasikitisha halafu inawakera walio wengi.

Kwangu binafsi, ‘picha nzima’ inayoonekana sasa, kwa wabunge wa CCM kuizungumzia serikali (eti) kwa kigezo dhaifu cha baada ya Uchaguzi Mkuu, siasa zinahamia bungeni, ni mfano halisi wa fikra zilizoganda. Kunahitajika mabadiliko makubwa.

Umefika wakati wabunge wa CCM watambue kwamba kukosoa utendaji na watendaji wa serikali si ishara ya chuki dhidi ya serikali iliyopo madarakani, bali ni utekelezaji wa wajibu muhimu utakaoisaidia (serikali) itende kwa kadri ya matarajio ya umma, na chama kiendelee kushinda.

Inapotokea Mbunge anakuwa mfano wa mzazi ambaye mtoto wake anajihusisha na vitendo viovu, badala ya kumkanya na kuionyesha jamii inayomtambua, kwamba hakubaliani na vitendo hivyo, yeye anamlinda, anamkingia kifua, anaiangamiza familia husika.

Kwa mantiki hiyo, hata wabunge wanaotokana na CCM, wanaposimama hadharani, tena ndani ya chombo cha uwakilishi mpana wa umma wa Watanzania walio zaidi ya milioni 40 katika hesabu yao, wakajidhihirisha kwa utetezi badala ya kuisimamia, kuihoji na kuishauri serikali, hawakitakii mema chama hicho.

Kwa maneno yao, wanaipotosha, wanaipoteza serikali na kwa hali hiyo, ikizidi kushindwa kutimiza wajibu wake kwa umma, watendaji waliopo serikalini hawaadhibiwi na umma, bali chama kilichopo madarakani. Chama Cha Mapinduzi.

Shauri yenu!

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa ambaye hivi sasa yupo bungeni mjini Dodoma. Anapatikana kwenye simu namba +255 745 691540, 0716635612 ama barua pepe;mgeta2000@yahoo.com.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment