Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ukizaa mtoto wa baba wa wizi si atakuona mama ni mhuni?

24th June 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, tuongee kidogo kuhusu watoto wanaozaliwa kwa wizi nje ya ndoa kama anavyotoa maoni mmoja wa wasomaji wetu kutoka ukanda wa Kaskazini na kama nawe utakuwa na maoni uyatume kwa ujumbe mfupi wa simu inayoonekana mwishoni mwa makala haya.

Naam. Msomaji huyu anaanza ujumbe wake ambao umerekodiwa katika ujumbe mbili tofauti kama ifuatavyo;

“Anti nakusalimu kwa jina la Bwana. Ninaposoma makala zako za kila Jumapili huwa machozi yananitoka.

Najiuliza kwanini wanawake wanashindwa kujiheshimu na kujifunza wakiwa wasichana na umri unapowakuta wanaaza kuviziwa wanaume wa watu na kujiachia ili wazae kwa tamaa ya kujengewa nyumba au kufunguliwa biashara hata kununuliwa magari?

Anti, katika familia nyingi hasa ukanda wa Kaskazini ni tabia iliyojengeka sana kwa baadhi ya wanawake kuzaa na waume za wanawake wenzao. Najiuliza; hivi ukizaa mtoto wa baba wa wizi si anakuona mama kuwa mhuni?

Mtoto huyu si angependa naye kulelewa na baba na mama waliomzaa na siyo walezi. Na je, unayemwibia mume anapolia kila siku Mungu muumba haoni?

Anti nataka utoe mada hii maana wanatakiwa kujua kuwa Mungu hashindwi na uchawi. Wanawapumbaza wanaume kwa madawa ya kienyeji wakijiona washindi. Mwisho wao Mungu atawahukumu.

Mimi nadhani mtu akijituliza atapata mume. Je, wanaovuruga ndoa za wengine wataishi milele? Ziko ndoa nyingi zilizovunjwa wa wadaku wa aina hiyo lakini wakae wakijua kuwa iko siku Mungu atawauliza. Wadau hawa mara nyingi wana kiburi na maneno machafu vinywani mwao kama vile wanayo haki ya kufanya usaliti huo dhidi ya wanawake wenzao.

Nimesema hayo yote kwa sababu mimi ni miongoni mwa kinamama hao wanaoibiwa mchana kweupe lakini navumilia kwani naamini Mungu ana visasi vyote. Mimi ni mwathirika mkuu kwa maana kama siyo watoto nisingekuwa hai. Wanaume zetu wamelishwa madawa ya kienyeji na matokeo yake hawasikii kitu sawa na mtu anayempigia mbuzi gitaa huku yeye anaendelea kutafuna na kucheua majani yake. Unakuta hawa wanawake hawana mtu mmoja. Je, ukimwi utatuacha jamani? Wapo wanawake walioweka hela mbele kuliko Mungu, hasa katika mikoa ya kanda ya Kaskazini.

Tujiulize, hawa watoto wanaozaliwa kwenye ndoa za watu kweli watakuja kuelewana? Na je, jamii inayokuzunguka na hata wazazi wanakuonaje unapozaa na mume wa mtu? Hata ukiwa na mihela ni bure maana huna heshima kwa jamii. Huyu Mungu ipo siku atatufuta machozi yetu na kugeuza kibao walie wao wanaodhulumu ndoa za wenzao.

Mimi Namuita Mungu kila dakika. Nampenda Mungu na naamini yote yana mwisho. Hata walivyovipata kwa njia ya uonevu vitaangamia. Mungu akubariki Anti uendelee kulea watu kimaadiili maana hata watoto wetu watajifunza”.

Mpenzi msomaji, hivyo ndivyo msomaji wetu huyu anamaliza ujumbe wake aliotuma kwa awamu mbili kupitia simu ya kiganjani akizungumzia kinamama wanaodowea waume za wanawake wenzao kwamba wamuogope sana Mungu kwa kuzitesa familia zisizo na hatia huku zikijawa na hofu ya maisha pasipo sababu.

Upo msemo kwamba “ukiona mtu mzima analia, ujue yamemfika makubwa. Msomaji huyu aliyelete ujumbe huo hapo juu, amevumilia baada ya kuona usaliti unaofanyika ndani ya ndoa yake na kuamua kuvunja ukimya. Hicho ndicho kinachotakiwa badala ya kuendelea kuwa kimya huku unaumia.

Wataalamu wa masuala ya saikolojia wanasema kwamba unapokuwa na tatizo fulani ukanyamaza kimya, tatizo hilo litaendelea kukutesa sana rohoni.

Lakini unapoeleza tatizo hilo kwa watu wengine unaowaamini, utajikuta unapata nafuu kimawazo kwani tayari wengine wanalijua na ama watakupa ushauri au watakusaidia kulipatia ufumbuzi. Kwa mantiki hiyo, kila anayetoa tatizo lake kwa mwingine aelewe kwamba japo ufumbuzi haujapatikana lakini tatizo limefahamika kwa wengi na majibu mbalimbali yatapatikana toka kwa waliosikia kilio cha mwenye tatizo.

Hapa nataka nimwambie msomaji wetu aliyetueleza juu ya wale kinamama wanaodowea waume za watu kwamba ujumbe wake sasa umewafikia watu wengi baada ya kuchapishwa gazetini na hivyo asubiri maoni, ushauri toka kwa wasomaji wengine.

Naam. Hili la mtu kumvizia mume wa mwenzake na kuamua kuzaa naye, limeziumiza familia nyingi. Ni nadra(mara chache) mume wa mtu kuzaa na mke wa tu na ikibainika hivyo. Yule mke kama ni wa ndoa huvunjika. Lakini wengine katika kulinda ndoa zao, ikitokea amechombeza na mume wa mtu, ndio hao huamua kuua kiumbe hicho kufuta ushahidi.

Lakini kwa upande wa wanaume, pia ni mara chache kwa mfano anazaa na mke wa mtu mwenye ndoa labda kwa wale wanaoishi bila ndoa japo wamezaa ambapo wanapobanwa, huamua kuachika ili aweze kumuegemea huyo mume wa mtu pengine kutokana na ahadi kama vile kujengewa nyumba, kuanzishiwa biashara, kununuliwa gari na kadhalika.

Lakini wanaoumia zaidi ni wale kinamama wenye ndoa zenye wanaume jeuri waliojaa viburi vya mali ambapo hutafuta mahusiano ya nje na kufikia hatua ya kuzaa nje ya ndoa, jambo ambalo ni kuvunja sheria za kidini na sheria ya Mwenyezi Mungu.

Ni ukweli usiopingika kwamba wapo baadhi ya kinamama wenye roho katili ambao wakimnasa mume wa mwanamke mwenzao hawamwachi. Wapo wanaozaa na wanaume wa watu kwa bahati mbaya na hawarudii tena kosa hilo.

Lakini wapo ving’ang’anizi ambao huingia hata kwenye ndumba(waganga) ili kupumbaza wanaume za wenzao na matokeo yake wanaume hawa wanakuwa hawaoni wala hawasikii. Wanaume wengine kwa kukolewa na madawa wakati mwingine pasipo kujua, huwafanyia visa wake zao ikiwa ni pamoja na kutowapa matumizi ya nyumbani, kuwatimua kwa mikwara na kadhalika.

Hata hivyo, wengi wetu tunaamini kuwa malipo ni hapa hapa duniani na kisasi Mungu muumba amesema tumwachie yeye mwenyewe. Kwa machozi ambayo kinamama wengi wanalia baada ya ndoa zao kutifuliwa, iko siku Mungu atatoa majibu hadharani ya walimwengu washuhudie. Hakuna kinachomshinda Mungu muumbaji.

Naam. Waliochangia mada iliyopita wanasema; “Mimi namshauri huyo dada na hali alishatolewa mahari na ujauzito juu, yeye atulie tu ajifungue, alee mwanae atapata mwenzi ampendaye tu na watafunga ndoa. Kama hatajali tuwasiliane nimpe mifano mingi inayofanana na ishu yake(Ally wa Dar 0713873565).

Naitwa Japhet wa Mwananyamala nampa pole huyo dada. Namshauri azidi kumtanguliza Mungu mbele kwani hata mimi hayo yalinitokea.

Ukiwa tayari kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment