



Tumekuwa taifa la kuomboleza. Kila wakati majanga mengi yanatupata na kupukutisha maisha ya watu wetu, lakini hatujifunzi na wala hatukumbuki kufiwa baada ya kitambo kidogo tu.
Ukitazama kwa kina idadi za ajali za majini, barabarani na ubora wa vyombo vya usafiri vinavyotumika hakika utakugundua kuwa mara nyingi tunajitakia majanga haya.
Juzi boti ya abiria ya mv Skagit ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ilizama umbali wa km kama 20 hivi kutoka Bandari ya Malindi, Zanzibar, na habari za mpaka jana zinasema kiasi cha watu 150 hivi ndiwo tu walikuwa wameokolewa kati ya abiria na wafanyakazi wa boti hiyo wanaofikia 290.
Maiti kama 34 imekwisha kupatikana. Hili ni janga kubwa, serikali imetangaza kupeperushwa kwa bendera nusu mlingoti kwa siku tatu na vikao vya Bunge vimehairishwa kwa muda kuruhusu wabunge kushiriki katika maombolezo.
Nasi tunaungana na waombolezaji wengine kuwapa pole ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa wao katika janga hili, pia tunawapa pole walionusurika.
Janga hili linatokea miezi tisa tu baada janga jingine lililotokea kisiwani Zanzibar, kwenye rasi ya Nungwi ambako Septemba 10, mwaka jana watu 1,529 walikufa na 941 kuokolewa na wengine zaidi ya 1,000 kutoweka baada ya meli ya Mv Spice Islanders kupinduka na kuzama katika mkodo wa Nungwi, Zanzibar.
Meli hiyo ilizama kutokana na kuzidisha abiria na mizigo; kitendo kilichosababisha viongozi kadhaa wakiwemo maofisa na vigogo wa Shirika la Bandari na Mamlaka ya Usafiri Baharini kusimamishwa na kufunguliwa mashitaka ya uzembe na kusababisha vifo.
Tukio jingine baya la ajali ya meli lililotikisa nchi hii ni lile la Mei 21, 1996 katika ziwa Victoria, mkoani Mwanza, ambalo meli ya Mv Bukoba ilipata ajali kwa kuzama, takribani watu 1,000 walipoteza maisha katika ajali hiyo. Meli hiyo ilikuwa imetoka Bukoba.
Tunayataja haya tu kwa kuwa ni matukio makubwa yaliyopindukia kwa idadi kubwa ya vifo, lakini yapo matukio mengine mengi, ni kama ni jambo la kawaida kusikia meli au boti imezimika baharini, kuzama na kuua watu. Wiki iliyopita tu meli iliyokuwa inapeleka mafuta ya dizeli kisiwani Mafia ilishika moto baada ya kutokea hitilafu.
Majanga haya pamoja na ya ajali za barabarani kwa hakika yameteketeza watu wetu, kiasi kwamba maswali magumu yasiyokuwa na majibu yamekuwa yanaulizwa, kwamba hizi ni ajali za kawaida tu au ni za kujitakia?
Ukitafakari kwa kina sana sisi ni mabingwa wa kuomboleza na kujiapiza kila tunapopatwa na janga kama hili la mv Skagit, lakini baada ya kitambo kidogo tu tunasahau machungu yote na kurudi kuendesha mambo kwa mazoea ambayo umakini hauna nafasi.
Tangu kuibuka kwa habari ya ajali ya mv Skagit juzi mchana, tumekuwa tunajiuliza maswali mengi; moja, juu ya utayari wetu katika kukabiliana na majanga kama haya; lakini la pili na lenye nguvu zaidi ni kwa kiwango gani vyombo vyetu vya usimamizi viko macho kulinda na kusimamia shughuli zote za usafiri baharini.
Itakumbukwa kwamba katika janga la mv Bukoba ni kana kwamba hakuna aliyewajibika kwa yaliyotokea, kila mmoja katika vyombo vyote vya kusimamia usalama wa meli alijiona hana sababu ya kuwajibika. Mambo yaliachwa hivyo kwa staili ya kuomboleza na kujiapiza tu, lakini uwajibikaji hakuonena hadi leo.
Pamoja na haya yote, itakumbukwa kwamba kwa sasa kuna mvutano juu ya usalama wa vyombo vya usafiri habarini vinavyosajiliwa Zanzibar, kama ambavyo imekuwa Tanzania Bara katika kusimamia kwa kina usalama wake; tunaelewa suala hili ni tete kwa kiasi fulani, lakini ni vema ikatiliwa maanani kwamba vyombo vyote hivi viliwili, yaani Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu Tanzania (Sumatra) kukaa kwa pamoja na kujadili kwa kina juu ya usalama wa vyombo hivi.
Haina maana yoyote ya kuomboleza kwa nguvu na kila aina ya vilio lakini kila baada ya kitambo kidogo tu tunasahau kuwa macho na makini katika usimamizi wa usalama baharini na hata nchi kavu, hivyo kurudi tena kwenye majanga yale yale.
Ni wakati sasa wakujifunza walau kwa makosa yetu wenyewe kama hata hatuwezi kujifunza kwa matatizo ya wengine. Tusikubali kuwa taifa la kuomboleza tu.