Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Usajili wa Simba, Azam FC uzingatie michuano ya CAF

18th June 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Baada ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufikia mwisho hivi karibuni, klabu za Simba na Azam zilimaliza katika nafasi za juu na hivyo kupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya mwakani ya klabu ya Afrika inayoandaliwa na shirikisho la soka barani, CAF.

Simba waliotwaa ubingwa wa ligi hiyo, watashiriki michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika huku Azam wakitarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho.

Baada ya ligi kumalizika, klabu zimeanza harakati za kusajili wachezaji wapya watakaoimarisha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao utakaoanza Agosti. Klabu za Simba, Azam na Yanga ni miongoni mwa zile zilizoripotiwa kila uchao kuhusiana na usajili wa nyota wapya.

Tangu harakati za kunasa nyota wapya zilipoanza, wachezaji kadhaa nyota wamekuwa wakitajwa kuwa wako katika mazungumzo na viongozi wa klabu hizo na wengine wakithibitishwa hadharani kuwa tayari wameshakubaliana na timu hizo na kusaini mikataba yao.

Kwakuwa dirisha la usajili halijafikia ukomo wake, sisi tunaona kuna haja ya kuwakumbusha viongozi wa klabu za Simba na Azam kuwa sasa zishirikiane vyema na maafisa wao wa benchi la ufundi katika kuunda vikosi imara vitakavyowapa nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya Afrika.

Tunawakumbusha kuangalia zaidi ushiriki wao katika michuano ya CAF na sio ligi kuu pekee kwa sababu haitakuwa jambo zuri kuziona timu hizi zikifanya vizuri katika ligi ya Bara, lakini zikiendelea kuliaibisha taifa kwa kuwa wasindikizaji wa michuano ya klabu bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Si jambo zuri pia kuona wenzetu wakifika mbali katika michuano ya klabu na hata kutwaa mataji mfululizo kama walivyofanya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika miaka miwili iliyopita huku sisi tunaowakilishwa na timu mbili za Bara na nyingine mbili za Zanzibar tukitumika kama ngazi ya mafanikio ya klabu za nchi nyingine.

Tunadhani itakuwa vizuri kama makocha wa Simba, Azam na klabu za Zanzibar zitakazotuwakilisha kwenye michuano ya CAF wakapewa nafasi ya kuimarisha vikosi vyao kwa mtazamo wa kiufundi zaidi, na sio kuingiliwa na viongozi wa klabu ambao timu ikivurunda hujiweka kando na kuwatupia lawama makocha.

Uwakilishi wa klabu zetu katika miaka ya hivi karibuni hauvutii sana. Kwa mfano, Yanga walitolewa katika raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya klabu bingwa miaka miwili iliyopita na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kufungwa nyumbani na ugenini kwa jumla ya magoli 4-2 na mahasimu wao Simba wakitolewa na Harass Al Hadoud ya Misri kwa magoli 7-3. Hata msimu uliofuatia baada ya hapo, Yanga waliaga mapema katika ligi ya klabu bingwa kwa kung’olewa na Zamalek ya Misri kutokana na kipigo cha jumla cha mabao 2-1.

Mwaka huu, Simba waliokuwa wakishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka huu, walijaribu kujitutumua kwa kuzitoa Kiyovu ya Rwanda na ES Setif ya Algeria, lakini mwishowe wakafungishwa virago na klabu ya Al Ahly Shandy ya Sudan.

Wawakilishi wa Zanzibar katika ligi ya klabu bingwa Afrika miaka miwili iliyopita, timu ya Mafunzo ilitolewa pia na The Gunners ya Zimbawe huku Miembeni ikitolewa kwa idadi kubwa ya mabao na Petrojet ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho. Matokeo ya kusikitisha kama hayo ndiyo yaliyozikuta timu nyingine za Zanzibar mwaka huu.

Kumbukumbu hizi mbaya katika miaka ya karibuni ndizo zinazotulazimu kuwapa rai viongozi wa klabu ya Azam inayojiandaa kushiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa na pia wakongwe, Simba kuwa wawe makini katika usajili wao.

Ikiwezekana, cheche za usajili wao mpya tuzione wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Affrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), itakayoanza Julai 14.

Simba, Azam na Yanga watakaoshiriki michuano ya Kombe la Kagame zinapaswa kuepuka usajili wa kishabiki unaoambatana na mazoea ya kuchukuliana wachezaji katika kila msimu. Badala yake, wasikilize ushauri wa kitaalam kutoka benchi la ufundi kwani kinyume chake watajikuta wakifanya vibaya na kuendelea kuwasononesha Watanzania.

Waseme inatosha kuwa wasindikizaji wa michuano ya CAF kwa kufanya usajili makini na kuandaa vikosi vyao mapema.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment