Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Muombeeni Rais Jk na Bunge:Prof. Tibaijuka

22nd July 2012
Print
Comments
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewataka Watanzania kumuombea Rais, Jakaya Kikwete, mawaziri pamoja na bunge ili wawe na hekima wakati wanapofanya maamuzi mbalimbali ya Taifa.

Profesa Tibaijuka amesema kuwa, bunge linahitaji hekima ya hali ya juu na kwamba kinyume na hapo ni kuchakachua sheria na mambo mbalimbali yanayohitaji maamuzi kwenye mhimili huo.

Alitoa kauli hiyo wakati wa kongamano la roho mtakatifu lililoandaliwa na Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam kupitia wakarismatiki ambao pamoja na mambo mengine jana wameliombea Taifa.

Kadhalika Profesa Tibaijuka ametaka Watanzania kuliombea taifa kuhusu mchakato unaoendelea wa kuandikwa kwa Katiba mpya usiwe wa chama au kikundi fulani bali kwa mustakabali wa taifa na vizazi vijavyo.

"Wasomi chuo kikuu wanasema unaweza kuandika Katiba viraka, sisi tusiruhusu hili, hekima inatakiwa katika uwandikwaji wa hili ili ilenge vizazi vijavyo" alisema.

Amewatahadharisha vijana wakati wanadai haki kwenye nchi yao watangulize mbele hekima lengo likiwa ni kutoivuruga amani ya taifa.

"Tunatakiwa tuombe kwa Mungu unyenyekevu, utii na kumcha Mungu ili tuweze kuwa na hekima, niwakumbushe taifa letu limebarikiwa toka lilipoanza linaamani na lipo katika bara ambalo nchi zake zinamatatizo hivyo tusiruhusu amani itoweke," alisema.

Naye, mbunge wa Mbinga Mashariki (CCM), Gaudence Kayombo ambaye alikuwa ameambatana na mke wake kwenye maombezi hayo alisema kuwa, endapo nchi ikipata watu wanaomjua Yesu, masuala ya wizi, uchakachuaji na matatizo ya ardhi hayatakuwepo.

"Nchi yetu haiwezi kuwa na watu wanaolalamika kila siku, tunatakiwa kupiga magoti na kuwaombea viongozi wetu wawe na hekima na maamuzi yanayompendeza Mungu," alisema.

Mratibu wa Karismatiki kanisa katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Estelatus Mtema kwa upande wake, alisema kuwa, kwa kiasi fulani karismatiki inafanya kazi zake na serikali na mara kwa mara imekuwa ikiliombea taifa.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment